Twahitaji tuishi kwa maadili ya dini ili kutatua baadhi ya changamoto zinazotukabili, asema Rais Kenyatta

0
(PSCU) – Rais Uhuru Kenyatta amewahimiza Wakenya kuzingatia kikamilifu maadili ya kidini ili kukabiliana na baadhi ya changamoto zinazokumba Taifa hili kama vile ufisadi.
Rais Kenyatta alisema kwamba iwapo Wakristo wangeishi sawa, kuwahurumia maskini na kuzingatia mafundisho ya biblia, hakungekuwa na ufisadi na maovu mengine yanayohusiana na rushwa hapa nchini.
“Iwapo tungeishi kulingana na biblia, tungeheshimiana. Na iwapo tungeishi kulingana na mafunzo tuliyopokea, tungeweza kusameheana ili kuwa na nchi yenye uwiano”, kasema Rais Kenyatta.
“Sisi sote tunafahamu changamoto zinazotukabili, hebu tuzitatue kwa kuishi kila siku kwa njia inayostahili Wakristo,” kaongeza Rais.
Rais Kenyatta alisema haya katika uwanja wa Nairobi Club jana jioni alipoongoza dhifa ya jioni ya mchango wa kusaidia kutafsiri Biblia kwa lugha nyingi zaidi za hapa nchini na kuwezesha Wakenya wote kuisoma kwa lugha ya mama.
Kulingana na Kasisi Peter Munguti, Mkurugenzi wa Kitaifa wa Shirika la Utafsiri na Uwezo wa Kusoma Biblia, biblia imetafsiriwa kikamilifu kwa lugha 21 kati ya lugha 60 za humu Nchini.
“Mradi huu ni muhimu kwa sababu utawezesha kila Mkenya bila kujali alikozaliwa kupata nafasi ya kusoma biblia kwa lugha inayogusa roho zao”, kasema Rais Kenyatta wakati wa hafla hiyo ya mchango iliyoandaliwa na Naibu Rais William Ruto, Shirika la Biblia Nchini na Shirika la Utafsiri na Uwezo wa Kusoma Biblia.
Akikariri kwamba aliahidi kutetea na kulinda Katiba ya Kenya, Rais Kenyatta alisema kwamba Kenya ni nchi inayomcha Mungu na akatoa wito kwa Wakenya kuheshimu imani ya kidini ya kila mmoja kama njia ya kuleta umoja na mshikamano wa kitaifa.
“Sisi ni taifa linalofahamu kwamba tuna rangi mbalimbali, jamii nyingi, dini nyigi na taifa la kustahimiliana”, kasema Rais Kenyatta.
“Hii ndiyo sababu nina furaha kuona wengi kutoka dini mbali mbali hapa wakiunga mkono mpango huu kama tutakavyounga mkono mipango yao kwa sababu taifa letu ni la kustahimiliana.
Hivyo ndivyo tunatarajiwa kutenda ili kuimarisha ustahimilivu na kukubaliana”, Rais alikariri.
Naibu Rais alisema yeye alinufaika na Biblia iliyoandikwa katika lugha ya Kikalenjini na akatoa wito wa kusaidia kutoa neno la Mungu kwa Wakenya ambao hawana Bibilia zilizotafsiriwa katika lugha zao asili.
“Ninaposimama hapa hii leo nilinufaika na Biblia iliyoandikwa katika lugha ya Kikalenjini.
Ni Biblia iliyoandikwa katika lugha ya Kikalenjijini iliyomfanya Babangu kusoma Neno la Mungu na kuacha alichokuwa akifanya, akamuoa mamangu na kutupeleka shuleni,” kasema Naibu Rais.
Akimnukuu shujaa wa ukombozi na Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela, Naibu Rais alisema, “Ukiongea na mtu katika lugha anayofahamu, ujumbe unaingia akilini mwake. Lakini ukizungumza na mwanamume au mwanamke  kwa lugha yake, ujumbe unaingia moyoni.”
“leo tuko katika wakati huo. Tunataka neno lihubiriwe katika lugha ambayo inaingia moja kwa moja katika mioyo ya Wakenya wengi ambao leo hii hawana Biblia iliyoandikwa katika lugha zao,” kaongeza  Naibu Rais.
Naibu Rais alisema kwamba katika ziara zake kote nchini ametambua kwamba baadhi ya changamoto zinazokumba taifa sio hasa za kiuchumi wala kisiasa bali ni za kiroho.
“Na hakuna tiba nyingine kwa matatizo ya kiroho. Huwezi kuyatibu kwa kutumia pesa. Huwezi kuyatibu kwa kutumia wadhifa. Unaweza tu kuyatibu kwa kufahamu Neno la Mungu kama mlivyoambiwa,” kasema Naibu Rais.
Katika mahubiri yake Kasisi Dkt. David Oginde, ambaye ni Askofu Msimamizi wa CITAM, alimpongeza Rais Kenyatta kwa kutangaza kwamba hatatia saini Mswada wa Mwaka 2018 wa Tume ya Wafanyikazi wa Bunge unaowapa marupurupu mengi.

Comments

comments

Share.

About Author

Chris is a digital nomad and travel the country while freelancing and blogging. Rest assured, his job is always his first priority.